
Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere, Prof. Penina Mlama, amesema kuwa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu imeongezeka kutoka nyanja mbili za awali riwaya na ushairi hadi kufikia nyanja nne ambazo ni riwaya, ushairi, vitabu vya watoto na tamthilia.

Awali akizungumza jijini Dar es Salaam Februari 17, 2026 katika hafla ya uzinduzi wa vitabu vilivyoshinda tuzo hiyo Prof. Mlama amesema mwitikio wa waandishi bunifu kushiriki umekuwa mkubwa na ndio maana nyanja hizo zimeongezeka ili kupanua wigo wa waandishi kushiriki.

Profesa Mlama ameeleza kuwa mwaka 2024/2025 washiriki 31 walijitokeza kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani, pamoja na Watanzania walioko nje ya nchi kama Ujerumani, Austria na Czech Republic huku usawa wa kijinsia ukiendelea kuimarika, wanawake wakifikia asilimia 33.3 ya washiriki mwaka 2025.

Akizungumzia muundo wa zawadi, Profesa Mlama alisema washindi hupokea fedha taslimu ambapo mshindi wa kwanza hupata shilingi milioni 10, wa pili milioni 7 na wa tatu milioni 5. Mbali na fedha, mshindi wa kwanza katika kila nyanja hupata muswada wake kuchapishwa na kusambazwa shuleni na maktaba za taifa.

Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi bunifu ina lengo la kutambua na kuzawadia uandishi bunifu kitaifa ni kukuza lugha ya Kiswahili, kuimarisha kikosi cha waandishi wa Tanzania, kuendeleza utamaduni wa kusoma na zinachangia kuhifadhi historia na mitazamo ya taifa pamoja na kukuza sekta ya uchapishaji wa ndani.


