
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi, amesema kuwa ujenzi wa Kampasi 16 za vyuo vikuu nchini kupitia Mradi wa Mageuzi ya Elimu ya Juu kwa Uchumi (HEET) unalenga kupeleka fursa za elimu ya juu na hasa elimu ya ujuzi katika maeneo ya pembezoni.

Akizungumza Februari 15, 2026 Mkoani Tanga, Prof. Mushi ameeleza kuwa kampasi hizo zitawezesha vijana kupata maarifa yanayohusiana moja kwa moja na mazingira ya kiuchumi ya maeneo husika, na hivyo kuchochea maendeleo ya jamii.

Prof. Mushi aliongeza kuwa kampasi mpya zitasaidia kupokea wimbi kubwa la wanafunzi wanaohitimu sekondari kufuatia mafanikio ya mpango wa Elimu bila ada, sambamba na kuandaa walimu wa amali na kada nyingine muhimu baada ya mabadiliko ya sera na mitaala.

Aidha, alibainisha kuwa ujenzi wa kampasi unatoa ajira za muda mfupi kwa wananchi, na mara chuo kitakapoanza kudahili wanafunzi Oktoba 2026, kitazalisha ajira za muda mrefu kwa wakazi wa maeneo husika.

Akifafanua zaidi, Prof. Mushi alisema kampasi hizi zitakuwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwani zinahusisha ujenzi wa barabara, upatikanaji wa umeme na maji, na kuongeza thamani ya ardhi inayozunguka maeneo ya vyuo.

Amesema kuwa idadi ya wanafunzi na wafanyakazi itafikia kati ya 5,000 hadi 7,000 ndani ya miaka mitano hadi kumi, hali ambayo itahitaji huduma zote za kijamii za miji midogo na hivyo kuwa fursa kubwa kwa wananchi wa Mkinga na maeneo mengine yanayojengwa kampasi mpya.


