Ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu Mzumbe katika eneo la Gombero wilayani Mkinga mkoani Tanga umeelezwa kuwa ni hatua muhimu ya kuimarisha fursa za upatikanaji wa elimu ya juu na kuchochea maendeleo ya Ukanda wa Kaskazini Mashariki.



Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir Februari 15, 2026 wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujejzi wa kampasi hiyo ambapo amesema itaongeza udahili na kuongeza rasilimali watu wenye ujuzi wa sekta mbalimbali, hivyo kuunga mkono mageuzi ya kiuchumi na maendeleo endelevu ya Taifa.



Naibu Waziri ameongeza kuwa Ujenzi wa Kampasi hiyo ni hatua inayolenga kusogeza elimu ya juu karibu zaidi na wananchi na kubadilisha taswira ya sekta ya Elimu nchini na amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi thabiti na maono ya kuifanya elimu ya juu kuwa nyenzo ya mageuzi ya kiuchumi. Pia ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuwezesha utekelezaji wa mradi huo muhimu.



"Wizara imejidhatiti kusimamia mradi kwa kuzingatia thamani ya fedha, ubora na muda uliopangwa, huku ikimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ili kuhakikisha uwajibikaji na tija inayokusudiwa inafikiwa," amesisitiza Naibu Waziri Wanu.