Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, ameeleza kuwa Tanzania inahitaji wataalamu wengi zaidi katika nyanja za sayansi na teknolojia ili kuendana na kasi ya maendeleo ya dunia.



Akizungumza jijini Dar es Salaam, Prof. Mkenda alisisitiza kuwa teknolojia ni matokeo ya matumizi ya sayansi, hivyo serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuandaa wataalamu kupitia programu ya Samia Scholarship Extended.



Amesema Mpango huo unalenga kuongeza idadi ya wataalamu wa fani muhimu ikiwemo Data Science, Artificial Intelligence, Allied Sciences na Sayansi ya Nyuklia, ambapo wanafunzi wa shahada ya kwanza na uzamili wanapatiwa ufadhili wa masomo ndani na nje ya nchi.



Prof. Mkenda amebainisha kuwa kuanzishwa kwa ufadhili wa masomo ya Sayansi ya Nyuklia ni kutokana na uwepo wa madini ya urani nchini na umuhimu wake katika tiba na kilimo.



Ameongeza kuwa tayari wanafunzi wa shahada ya uzamili wameanza kusomea fani hiyo nje ya nchi na wanafunzi bora wa shahada ya kwanza watapelekwa kusomea nje ya nchi katika vyuo vikuu mahiri.



Aidha, Prof. Mkenda ameaguza michakato ya uteuzi wa wanafunzi Kwa ajili ya ufadhili uzingatie haki na ufaulu wa juu bila upendeleo wa sura, jinsia au kabila.