Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza vipaji vya sayansi ili kufikia maendeleo endelevu ya taifa.



Akizungumza Januari 30, 2026 Jijini Dar es Salaam wakati wa kuwaaga Vijana 16 wanaokwenda masomoni nchini Afrika Kusini chini ya Ufadhili wa Samia Skolashipu Extended DS na AI+, amesisitiza kuwa sayansi na teknolojia ni nguzo kuu za maendeleo ya taifa na kwamba Serikali imejipanga kutoa fursa za masomo na mafunzo ndani na nje ya nchi kupitia programu mbalimbali.



Amewataka wazazi na Wanafunzi kuzifahamu fursa za masomo katika nchi mbalimbali Duniani, hivyo amewahimiza wanafunzi wenyewe uwezo katika Sayansi na kitaaluma kuendeleza vipaji vyao.



Aidha, Prof. Mkenda amesema kuwa, pamoja na jitihada za Serikali bado kuna changamoto ya uhaba wa walimu wenye ujuzi wa kutosha katika fani za sayansi, jambo linalohitaji uwekezaji mkubwa katika mafunzo ya walimu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kujifunza na kutoa nafasi kwa walimu kupata mafunzo ya kitaalamu ili kuendana na mahitaji ya dunia ya sasa.

Ametoa wito kwa wadau wote, zikiwemo taasisi za elimu kushirikiana na Serikali kusaidia wanafunzi wenye changamoto mbalimbali ili wasiachwe nyuma.