
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) CPA. Antony Kasore amesema kuwa dhamira ya VETA ni kuweka mfumo nyumbufu wa mafunzo unaowezesha Watanzania kupata elimu ya ufundi kwa usawa na ubora unaokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

Amesema hayo Januari 24, 2026 katika Wilaya ya Chemba wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo ilipofanya ziara katika Chuo cha VETA Chemba ambapo amesema kuwa utekelezaji huo umeleta mafanikio ikiwemo ongezeko la udahili wa wanafunzi, mafunzo kwa wajasiriamali zaidi ya 6,500, marejeo ya mitaala 126, na ujenzi wa vyuo vipya 29 nchini, ikiwemo Chuo cha Chemba chenye wanafunzi 130 waliodahiliwa.

CPA Kasore pia ameeleza kuwa serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeendelea kuboresha vyuo vya VETA kwa kuvipatia mitambo na vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na kuboresha miundombinu ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia ya kisasa.


