
Ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya Vyuo vya VETA pamoja na uwekaji wa mitambo na vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia umeonyesha juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunzia katika Vyuo hivyo.

Mhe. Husna Sekiboko, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo amesema hayo Januari 24, 2026 wilayani Chemba wakati wa ziara ya Kamati hiyo katika Chuo cha VETA Chemba ambapo amesema ndani ya muda mfupi vyuo vimeboreshewa miundombinu ya ufundishaji na ujifunzaji hatua inayoonyesha umakini katika utoaji wa mafunzo kwa vitendo yanayoendana na teknolojia ya kisasa.

Ameeleza kuwa awali Vyuo hivyo vilikuwa na vifaa vichache vya kutolea mafunzo kwa vitendo hali iliyoleta changamoto ya kutoa mafunzo hayo kwa ufanisi na kuwezesha wanafunzi kupata ujuzi wa vitendo. Ameongeza Mabadiliko yaliyofanyika yameondoa changamoto hiyo na kuvifanya Vyuo vya VETA kuwa na mazingira yanayokidhi mahitaji ya mafunzo ya ufundi stadi.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amesema kuwa Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika kuboresha mazingira ya kujifunzia katika vyuo vya VETA.

Amebainisha kuwa vifaa vya kisasa vilivyowekwa katika Vyuo 53 vya VETA vimewapa wanafunzi ujuzi unaowawezesha kujiajiri na kuendana na mahitaji ya soko la ajira, na kwamba Serikali huku ikiendelea kuboresha Vyuo vilivyobaki ili mafunzo ya vitendo yawe ya ubora na viwango cha juu.

Mhe. Ameir ameongeza kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado kuna haja ya VETA kuendelea kujitangaza kwa umma na kutoa kozi zinazoendana na mazingira na mahitaji ya maeneo husika.

Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa Serikali inaendelea na dhamira ya kuboresha vyuo vya VETA ili kuhakikisha kila vijana wanapata nafasi ya kushiriki na kunufaika na mafunzo ya ufundi stadi, bila kuachwa nyuma.

