
Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika elimu umezingatia ubora wa elimu, usawa wa fursa, ubunifu, na matumizi yanayolengwa ya teknolojia za kidijitali Nchini.

Kauli hiyo imetolewa Januari 14, 2026 jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi akizungumza katika Warsha ya kujenga uelewa wa pamoja juu ya Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika Elimu na Miongozo yake.

Miongozo hiyo ni pamoja na Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika Elimu 2024/25–2029/30, Mwongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika Shule na Vyuo vya Ualimu na Mwongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika Vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi.

Mingine ni Mwongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika Vyuo Vikuu na Mwongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Akili Unde katika Elimu. Amehimiza ushirikiano na wadau ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

