Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema kuwa Miongozo ya Kitaifa ya Elimu ya Kidijitali kwa ngazi zote za elimu na Mwongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Akili Unde (AI) katika Elimu inatoa mwelekeo wa namna taasisi zinavyoweza kutumia teknolojia za kidijitali na AI katika ufundishaji, utafiti, tathmini na utawala.



Prof. Nombo ameeleza hayo Januari 14, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua Warsha ya kujenga uelewa wa pamoja juu ya Mkakati huo na Miongozo yake, akisisitiza kuwa mabadiliko ya kidijitali si chaguo tena, bali ni hitaji la lazima katika elimu, ili kuzalisha nguvu kazi mahiri.



Katika kufanikisha azma hiyo, amewataka walimu na waelimishaji kutumia kikamilifu teknolojia katika kufundishia na kujifunzia ili kwenda sambamba na mabadiliko yanayojiri duniani katika nyanja hiyo.



‘’Vyuo vya ualimu, vyuo vikuu na taasisi zote za mafunzo zinapashwa kuzingatia ufundishaji wa kidijitali, ujumuishaji wa TEHAMA, uelewa wa Akili Bandia (AI), pamoja na stadi za data katika programu za mafunzo ya awali na mafunzo kazini’’ amesema Prof. Nombo.