
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa Serikali inatekeleza Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) wenye thamani ya takriban Sh. trilioni moja, unaokwenda kuleta mageuzi makubwa katika elimu ya juu nchini.

Prof. Mkenda ameeleza hayo Disemba 20, 2025 Mkoani Lindi, katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa Kampasi ya UDSM Lindi. Amebainisha kuwa kwa kupitia mradi huo ujenzi unaendelea katika maeneo 47 nchini ikiwemo kampasi hiyo.

"Tuna ujenzi wa madarasa, kumbi za mihadhara na maabara 452, mabweni 26, pamoja na maabara na karakana 309 bila kusahau ufadhili wa masomo kwa wahadhiri wa byuo vikuu vya Serikali na Binafsi" amebainisha Waziri Mkenda.

Amesema mradi huo unakwenda kuongeza fursa kwa vijana wa kitanzania kupata elimu ya juu katika fani mbalimbali huku akisisitiza kuwa ptogramu zitakazotolewa zitajikita pia katika kutoa elimu na ujuzi.



