Serikali imewataka viongozi wa usimamizi wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi hiyo ili kulinda rasilimali za umma na kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana.



Akifungua mafunzo ya usimamizi wa ujenzi kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Elimu ya Awali na Msingi (BOOST), kwa niaba ya Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa ElimuMsingi, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolokia Abdul Maulid amesema ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zimebainisha mapungufu katika baadhi ya miradi, hivyo kila hatua ya ujenzi lazima ikaguliwe na wataalamu wa halmashauri.



Maulid alisisitiza hayo Oktoba 11, 2025 Mkoani Morogoro, amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila mtoto anajifunza katika miundombinu bora, hivyo miradi ya ujenzi lazima ifuate viwango vilivyowekwa.



Pia ameliwataka viongozi, shule na jamii kuanzisha utaratibu wa ukarabati mdogo kupitia ruzuku za uendeshaji ili kuzuia uchakavu wa mapema na kudumisha miundombinu.

Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Awali na Msingi kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI alieleza kuwa mafunzo hayo yanawahusisha washiriki 3,202 kutoka mikoa ya Morogoro, Iringa, Arusha na Mwanza, yakilenga kuboresha usimamizi wa miradi na kuhakikisha thamani ya fedha. Amesemw kuwa Serikali imetumia sh. bilioni 311.3 katika miaka ya fedha 2022/23 na 2023/24 kwa ujenzi na ukarabati wa shule, ikijumuisha madarasa, vyoo, mabweni, nyumba za walimu, majengo ya utawala na shule mpya 46