
Maonesho Maalum ya Ufadhili wa Masomo kutoka Urusi yamefanyika Oktoba 10, 2025, jijini Dar es Salaam katika Kituo cha Sayansi na Utamaduni wa Urusi yakihudhuriwa na wadau mbalimbali wa elimu.

Akimwakilisha Mkurugenzi wa Elimu ya Juu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bw. Clement Sanga amesema kuwa Maonyesho hayo ni jukwaa linalowaunganisha wanafunzi wa Kitanzania na wawakilishi wa Vyuo Vikuu 12 kutoka Shirikisho la Urusi likilenga kutoa taarifa sahihi na fursa za ufadhili wa masomo (scholarships) kwa wanafunzi wanaotafuta elimu ya juu nje ya nchi.

Ameongeza kuwa maonesho hayo hayataishia Dar es Salaam pekee, bali yataendelea pia katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela (NM-AIST) mkoani Arusha, ili kuwafikia wanafunzi kutoka Kanda ya Kaskazini na maeneo ya pembezoni.

Balozi wa Urusi nchini Tanzania Mhe. Andrey Levonovish Avetsyan ameasisitiza kuwa maonyesho hayo yanathibitisha dhamira ya Urusi kuwekeza katika rasilimali watu na kufungua milango ya elimu ya kimataifa kwa vijana wa Kitanzania


