
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda amezindua ugawaji wa vifaa vya kielimu na saidizi kwa walimu, wakufunzi na walimu tarajali wenye ulemavu vyenye thamani ya Sh. Bilioni 5.3.

Uzinduzi huo umefanyika Januari 05, 2026 jijini Dodoma, ambapo Waziri Mkenda amesema kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa sera na maboresho ya mitaala, na kwamba jitihada za uwekezaji zimewezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kupata elimu bora.

Waziri Mkenda amekumbusha alichosisitiza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania kuwa, Serikali inapotekeleza maendeleo jumuishi, itaendeleza jitihada zilizoanza za kuweka miundombinu na vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum katika ngazi zote za elimu.

Vifaa vilivyozinduliwa ni pamoja na kompyuta mpakato 688, mashine ya kidijiti ya kurekodi sauti 377, tabuleti 196, machine ya braille ya kielektroniki 19, emboza 6, machine ya kuongeza sauti 7 na seti 4 za kupima usikivu.

Vifaa hivyo vinasambazwa katika shule za Msingi 309, shule za Sekondari 629 na Vyuo vya Ualimu 10 kwa ajili ya waalimu, wakufunzi na walimu tarajali wenye mahitaji maalum katika halmashauri zote 184.

Wanufaika wa vifaa hivyo, ni wenye ulemavu wa viungo 342, wenye changamoto ya uoni 310, wenye uziwi 155, wenye ualbino 90, wenye usikivu hafifu 158, walimu tarajali 63 na wakufunzi 20 wenye ulemavu.


