
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo ameeleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa jengo jipya la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) linaloendelea kujengwa jijini Dodoma. Septemba 10, 2025 mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo.
Prof. Nombo amesema kuwa ujenzi umefikia asilimia 35, hali inayoonyesha umeenda mbele ya ratiba kwa asilimia 10 ikilinganishwa na lengo la awali la asilimia 25.
Mradi ulianza kutekelezwa mwezi Machi 2025 na unatarajiwa kukamilika Machi 2026; ukikamilika utakuwa chachu kubwa kwa vijana katika kukuza na kuendeleza ubunifu wao, hasa baada ya taasisi kuhamia Dodoma kutoka ofisi zilizopo Dar es Salaam kwa maelekezo ya Serikali.
Prof. Nombo amepongeza ubora wa ujenzi na kutoa wito kwa COSTECH kusimamia kikamilifu ubunifu wa vijana ili bunifu zinazozalishwa ziwe na viwango vinavyokubalika na kuweza kushindana kwenye masoko ya ndani na ya kimataifa. Mradi unakadiriwa kugharimu shilingi bilioni 7.3 hadi kukamilika na utakuwa na uwezo wa kuchukua watu 600 kwa wakati mmoja, jambo litakaloongeza fursa za mafunzo, uzalishaji na ajira kwa vijana.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, amesema taasisi ina wataalamu wa kutosha wanaowaelekeza vijana namna bora ya kukuza ubunifu wao, ikiwemo kuwasaidia kuanzisha kampuni changa, kuwasajilia, kuwalipia kodi na kuwawezesha kujiajiri pamoja na kuwaajiri wengine