
Kijana Joseph Joachim Mtei, mwenye ulemavu wa mikono na aliyemaliza masomo ya Ufundi Stadi katika Chuo cha VETA Dodoma, amekuwa mfano wa kuigwa baada ya kuwa na bidii na kupelekea kuajiriwa katika Kampuni Tanzu ya Ujuzi ya VETA.

Huu ni utekekezaji kauli mbiu ya hakuna mtoto kuachwa katika elimu na ujuzi kutokana na hali yeyote.

Uwezo wake na bidii vimewafurahisha wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, ambao wamemzawadia kiasi cha shilingi 1,600,000/= kilichochangwa na wajumbe hao.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Husna Sekiboko, alipokabidhi fedha hizo kwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amesisitiza kuwa Wizara na VETA imefanya jambo la mfano kwa kumpatia ajira kijana huyo ambayo imemwezesha kutumia ujuzi alioupata na kuthibitisha kuwa elimu ya ufundi stadi ni daraja la fursa na maendeleo.

Aidha, Kamati imetoa wito kwa Wizara ya Elimu kuendelea kutoa nafasi kwa vijana wenye ulemavu ili wapate ujuzi hatimae wachangie katika maendeleo ya taifa

