Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda na Naibu Waziri Mhe. Wanu Hafidh Ameir wamesisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu nchini.



Akizungumza walipowasili katika Ofisi za Wizara tarehe 18 Novemba 2025 jijini Dodoma, Prof. Mkenda ameeleza kuwa Wizara imejipanga kuhakikisha elimu inayotolewa inawawezesha vijana kupata maarifa, stadi stahiki na ujuzi ili waweze kujiajiri na kushindana katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.



Waziri Mkenda ameongeza kuwa Wizara itasimamia kikamilifu elimu katika ngazi mbalimbali na kuweka mkazo katika mafunzo ya amali.



Kwa upande wake, Naibu Waziri Mhe. Wanu Hafidh Ameir ameahidi ushirikiano katika kufanikisha mageuzi hayo na amehimiza kuendeleza utamaduni wa ushirikiano na weledi katika kazi ili kuhakikisha malengo ya Serikali ya kutoa elimu bora kwa wote yanafanikiwa.



Mhe. Wanu na Prof. Mkenda wamepokelewa rasmi katika ofisi za Wizara, ambapo watumishi wamewafurahia Viongozi hao na wameonesha ari ya kushirikiana katika safari ya mageuzi ya elimu