
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, tarehe 27 Novemba 2025, amepokea taarifa ya mwenendo wa utekelezaji wa Programu ya Samia Extended Scholarship DS/AI+. Programu hii inalenga kufadhili wanafunzi wa Tanzania Bara na Zanzibar kusoma katika vyuo vikuu mahiri duniani, katika fani za kimkakati za Sayansi ya Data, Akili Bandia (Artificial Intelligence), na Sayansi Shirikishi kwa mwaka wa masomo 2025/2027.

Akizungumza na Kamati ya Programu hiyo inayoongozwa na Prof. Makenya Maboko, Prof. Mkenda ameipongeza kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya. Aidha, amesisitiza ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha malengo ya programu yanatimia kwa manufaa ya taifa.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amewahimiza wajumbe wa Kamati na Viongozi wa Wizara na Taasisi kuendelea kushirikiana kikamilifu na kutekeleza maagizo ya Waziri ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa na programu hiyo.
Naye, Mshauri wa Kamati ya Programu, ambaye pia ni Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, ameishukuru Serikali kwa kuanzisha mpango huu wa kimkakati. Ameahidi kuwa COSTECH itaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha utekelezaji wa programu unakwenda sambamba na matarajio ya Serikali.

