
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amezindua rasmi mtaala na mafunzo ya ufundi wa aluminium na ufungaji vioo (Aluminium and Glass Fitting with Metal Fabrication), akisisitiza kuwa elimu ya ufundi inayozingatia ujuzi wa vitendo ni suluhisho la ajira kwa vijana nchini.

Uzinduzi huo umefanyika Aprili 23, 2026 jijini Dar es Salaam, ukiwa ni matokeo ya ushirikiano kati ya VETA na Aluminium Emirates Profile.

Akizungumza katika hafla hiyo, Ameir alisema hatua hiyo inaendana na dhamira ya Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha elimu inayozingatia ujuzi ili kuzalisha wahitimu wanaoweza kujiajiri na kuajiriwa kwa ufanisi.

Aliongeza kuwa mtaala huo mpya umeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya soko la ajira na mabadiliko ya teknolojia, huku ukiweka mkazo kwenye mafunzo ya vitendo.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Husseni Mohamed Omar, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za mafunzo na sekta ya viwanda ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa na ujuzi unaohitajika moja kwa moja kazini.

Naye Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) CPA Anthony Kasore amesema Ushiriki wetu kama VETA katika mpango huu na Aluminium Emirates Profile ni sehemu ya mkakati wa Mamlaka kuhakikisha mafunzo tunayotoa yanakidhi mahitaji halisi ya soko la sasa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Aluminium Emirates Profile, Degratius Marandu, kupitia ushirikiano huo, wakufunzi na mafundi watapata maarifa na teknolojia za kisasa zitakazowawezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuongeza ubora katika sekta ya ujenzi.


