April 13 mwaka 2024 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amekutana na kamati iliyoundwa na Wizara kuendesha Tuzo ya Uandishi Bunifu na Uongozi wa Taasisi ya Elimu Tanzania(TET) kujadili maandalizi ya Tuzo kwa Mwaka 2024.



Akizungumza na vyombo vya Habari baada ya kikao Prof. Mkenda amesema Tuzo hiyo inachochea uandishi nchini kwani tangu ianzishwe mwaka 2023 kumekuwa na mwamko mkubwa wa maandiko mengi kutoka kwa waandishi wa hapa nchini.



Amewataka Watanzania kuongeza ari ya usomaji na kuendeleza utamaduni wa kuandika vitabu"



"Tuzo hii ni hamasa kubwa ya uandishi hapa nchini kwani tangu ianzishwe imechochea waandishi wengine kuweza kuwasilisha maandiko mbalimbali ambayo mengi yanaonekana kuwa na maudhui bora yatakayo ongeza wigo wa vitabu vya kusoma hususan katika shule, vyuo na jamii kupitia Maktaba" amesema Prof.Mkenda.



Prof Mkenda ameongeza kuwa uandishi Bunifu ni sehemu ya kukuza na kuhifadhi lugha na utamaduni wa mtanzania ambayo imehimizwa katika Toleo la 2023 la Sera ya Elimu na Mafunzo na Mitaala mipya.



Amebainisha kuwa Mwaka huu kilele na utoaji Tuzo itakuwa tarehe 13 Aprili, 2024 jijini Dar Es Salaam na Mgeni Rasmi ni Mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Uandishi Prof AbdulRazak Gurnah.



Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo Prof. Penina Mlama amesema miswada zaidi ya 200 imepokelewa kutoka kwa watanzania katika kada tofauti tofauti.

"Tumeendelea na maadalizi hasa kwa upande wa kuchambua miswada iliyowasilishwa, Kwa sasa majaji wanasoma miswada yote na ndo wataamua washindi ni kina nani”. amesema Prof.Mlama.



Aidha Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt.Aneth Komba ameieleza kuwa tuzo hizo ni alama tosha ya kuonesha uwezo shindani uliopo kwa waandishi bunifu nchini.

Ametaja nyanja tatu zinazo shindaniwa kuwa Riwaya, Ushairi na Hadithi za watoto.