Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, ameielekeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha inaweka mifumo madhubuti ya kuwawezesha walimu kujiendeleza kitaaluma kupitia mafunzo kazini, ili waweze kuendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya sasa ya dunia.



Mhe. Majaliwa ametoa wito huo katika Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani Oktoba 04, 2025 mkoani Geita, akisisitiza kuwa mafunzo hayo yahusishe matumizi ya teknolojia ya kidijitali na yawafikie walimu wote ili kufanikisha ufundishaji na ujifunzaji wa kisasa.



Waziri Mkuu amesisitiza kuwa mafanikio ya taifa yanategemea ubora wa elimu, hivyo ametoa wito kwa viongozi wa dini, jamii, na wadau kushirikiana na Serikali kuboresha mazingira ya elimu. Pia, ameishauri CWT kushirikiana na waajiri na wadau kutatua changamoto za walimu.



Mhe. Majaliwa ameongeza kuwa Serikali, chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kusimamia utekelezaji wa sera na mikakati ya kuboresha elimu sambamba ba kuajiri walimu kila mwaka ili kupunguza uhaba wa watumishi na mzigo wa kazi mashuleni.