Ujenzi wa Kampasi ya Mzumbe katika eneo la Gomera Mkoani Tanga unaofadhiliwa na Benki ya dunia kupitia Wizara ya  Elimu, Sayansi na Teknolojia  umefikia asilimia 80.



Akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. William Mwegoha amesema ujenzi wa chuo hicho ulianza Julai 2021 na unatarajia kukamilika mwezi Mei 2026 lengo kuu likiwa kuongeza fursa za elimu ya Juu, kuboresha mazingira ya ujifunzaji na kuchochea ushiriki wa wahitimu wa vyuo vikuu katika kukuza uchumi.



Prof. Mwegoha amesema Mradi huo unatekelezwa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi ( HEET) na kwamba Chuo kimetengewa Dola za kimarekani Milioni 21 kwa ajili ya uboreshaji wa mazingira ya kufundishia na kujifunzia Kampasi kuu na kuanzisha Kampasi Mkoa wa Tanga.



Ujenzi wa kampasi ya Mzumbe ya Tanga unahusisha jengo la taaluma lenye madarasa 6 yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 60 kila moja, ukumbi wa mihadhara wenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 320, Maktaba, duka ka vitabu, ofisi, stoo na chumba cha mtandao.



Majengo mengine ni pamoja na Hostel mbili za wavulana na wasichana zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 180 kila moja, bwalo lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 450, kituo cha Afya, nyumba Nne za wafanyakazi na miundombinu ya majisafi na taka.



Prof. Mwegoha amemshukuru Rais Samia kwa kuridhia uanzishwaji wa Mradi wa HEET ambao umewezesha Chuo kupata fedha za kutekeleza shughuli mbalimbali zitakazochangia kuleta mageuzi makubwa katika utoaji wa elimu ya juu nchini ikiwemo kuwezesha Chuo kutekeleza majukumu yake ya kufundisha, utafiti na kutoa huduma za kitaaluma kwa ufanisi zaidi.



Kampasi ya Tanga ikikamilika itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,400 kwa mara moja.