Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Serikali inaendelea kuunga mkono juhudi za Taasisi ya Lalji Foundation katika kuimarisha sekta ya elimu na maendeleo ya kijamii, hususan katika kuhakikisha watoto wanapata elimu bora na jumuishi.



Akizungumza Januari 10, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya ugawaji wa vifaa kwa wanafunzi kutoka vituo vya kulea watoto yatima, Waziri Mkenda amesema Serikali inautambua na kuuthamini mchango wa taasisi hiyo katika ujenzi wa shule na utoaji wa misaada mbalimbali inayochochea maendeleo ya elimu nchini.



Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kutoa elimu bila ada kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita, pamoja na kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wenye uhitaji, ili kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa fursa ya elimu kwa sababu ya uwezo wa kifedha.



Aidha, Waziri Mkenda amesema Serikali imegawa vifaa vyenye thamani ya shilingi bilioni 5.3 kwa walimu na wanafunzi wenye mahitaji maalum, akibainisha kuwa kwa mara ya kwanza vitabu vyote kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita vinachapishwa kwa maandishi ya nukta nundu ili kuongeza ushiriki na ufanisi wa ujifunzaji