Rais wa Zanzibar na Mwenyekiri wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametoa wito kwa Bara la Afrika kuandaa nguvu kazi yenye ustadi na maarifa inayosimamia utamaduni na lugha za asili za Afrika.



Wito huo ameutoa Februari 21, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa ufungaji wa Kongamano la Kwanza la Kimataifa kuhusu Dhima ya Lugha za asili katika Kujenga na Kukuza Diplomasia ya Kiuchumi na Kiutamaduni kupitia hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda.



Mhe. Dkt. Mwinyi ameongeza kuwa bara la Afrika ndilo lenye idadi kubwa ya vijana duniani ambapo katika miaka michache ijayo, inasemekana kuwa Bara la Afrika litakuwa ndilo tegemeo la nguvu kazi ya dunia hivyo vyema kujiandaa kuikabili hali hiyo.



Kongamano hilo limeshirikisha wataalamu wa lugha na watafiti, wafanyabiashara wakubwa na wadogo, watu mashuhuri na Viongozi Wastaafu na mahiri katika kutumia lugha adhimu ya Kiswahili ikiwa ni miongoni mwa lugha za asili ambayo inazidi kupata mafanikio Duniani.