Na
WyEST
PWANI

Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga amewahimiza wasimamizi wa mradi wa Ujenzi wa VETA ya Wilaya ya Kisarawe na Chalinze kufuata Kanuni za Ujenzi wa Miradi hiyo na kukamilisha ujenzi hatua kwa hatua huku akiwataka kufanya marekebisho katika maeneo yenye Changamoto zilizobainika.



Mhe. Kipanga ametoa rai hiyo March17, 2024, akiwa katika ziara ya Kukagua na kufanya tathmini ya ujenzi wa VETA hizo ikiwa ni miongoni Mwa VETA 64 zinazojengwa na Serikali nchini.



Katika hatua nyengine Kipanga amemtaka Mhandisi, Mshauri Elekezi na Afisa Manunuzi wa Halmashauri zilizo na Miradi ya VETA kuwepo eneo la ujenzi wakati wote ili kuhakikisha mafundi wanajenga kwa ufanisi na kufuata taratibu zote za ujenzi.



"Nitoe wito kwa Halmashauri, Wilaya zote zenye miradi ya VETA watalamu hao watatu wawepo eneo la mradi kwa ajili ya kutoa msaada na ushauri kwa mafundi", alisisitiza Kipanga.



Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya Kisarawe Bupe Mwakibete kwa niaba ya Mkuu wa Wiyaya ya Kisarawe, Mhe Fatma Nyangasa ameishukuru Serikali kwa kutenga fedha za Ujenzi wa chuo cha VETA Kisarawe kinachojengwa eneo la Kazimzumbwi na kuahidi kusimamia kwa karibu ujenzi huo ili ukamilike kwa wakati na kwa ubora.