Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amekutana na ujumbe kutoka Benki ya Dunia uliongozwa na Meneja wa Masuala Elimu wa Kanda Afrika Mashariki na Kusini Bi. Muna Salih Meky kuzungumzia mageuzi mbalimbali ya Elimu Nchini ikiwemo utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 Toleo la 2023 na Mitaala Mipya ya Elimu.



Prof. Mkenda ameeleza kuwa serikali ya Tanzania imejizatiti kikamilifu kufanya mageuzi makubwa kuhakikisha inatoa Elimu bora kwa usawa na kutoa fursa za ujifunzaji kwa watu wote katika dhana ya maendeleo endelevu ya Taifa.



Mkenda amesema serikali inafanya uwekezaji wa miundombinu mbalimbali ya Elimu, ndio maana inahimiza ushirikiano na Wadau wa maendeleo kushiriki katika uimarishaji wa Miundombinu hiyo ikiwemo ya Elimu ya Amali inayopewa msukumo katika kuwezesha umahiri wa Vijana katika stadi mbalimbali za kazi kama Kilimo, Ufugaji, Tehama, Ufugaji, Uhandisi na nyingine.



Kwa upande wake Bi. Muna ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kufanya uwekezaji wa miundombinu na kuendelea kusimamia Elimu, na kwamba Benki ya Dunia itaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuhakikisha inafikia azma ya kuwaandaa Vijana wenye ujuzi kuwawezesha kujiajiri au kuajiriwa.