Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imepokea ujumbe wa wataalamu kutoka Falme ya Eswatini ambao wapo katika ziara ya mafunzo ya ulinganifu, inayoratibiwa na taasisi ya Economic Policy and Analysis Research Centre (ESEPARC) kwa kushirikiana na Wizara ya Kazi na Hifadhi ya Jamii (MoLSS) ya Falme ya Eswatini.



Ziara hiyo imeanza leo, tarehe 13 Oktoba 2025, ikiwa na lengo la wataalamu wa nchi hiyo, kupata uzoefu kutoka Tanzania wa utekelezaji wa programu za maendeleo ya ujuzi, ikiwa ni sehemu maandalizi ya mpango kabambe wa kukuza ujuzi katika Nchi hiyo.



Akizungumza na ujumbe huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, amesema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ina jukumu la kusimamia na kuratibu utoaji wa elimu nchini, kuandaa Sera, Sheria na miongozo mbalimbali kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi elimu ya juu. Lengo kuu likiwa kuandaa wahitimu wenye maarifa, stadi na ujuzi.



Aidha, Prof. Mushi amebainisha kuwa Wizara pia inasimamia maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu pamoja na kuimarisha matumizi yake katika sekta mbalimbali zikiwemo biashara, viwanda, kilimo na afya.



Ili kufikia malengo mkazo umewekwa katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata mafunzo ya kumjengea ujuzi utakaomwezesha kujiajiri au kuajiriwa, jambo linalochochea ukuaji wa uchumi na kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira.



Kwa upande wake, Bi. Gcebile Dlamini, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mipango na Maendeleo ya Rasilimali Watu kutoka Eswatini ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwapa fursa ya kujifunza njia bora za uendeshaji wa elimu na maendeleo ya ujuzi, kwani Tanzania imepiga hatua kubwa katika maeneo hayo