
Serikali imekabidhiwa rasmi majengo ya Shule ya Sekondari mpya Dkt. Samia iliyopo Iyumbu jijini Dodoma, ambayo imegharimu Shilingi bilioni 17.8.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Septemba 26, 2025 jijini Dodoma, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Rasilimali Watu katika Wizara hiyo Ndug. Fredrick Kayombo, amesema kuwa amekagua majengo yote na kwamba ameridhishwa na kazi iliyofanyika kuwa ni ya ubora na viwango.
‘’Tunaipongeza Serikali chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa katika Shule hii ya mfano, iliyoyosheheni miundombinu bora na ya kisasa. Ni wajibu wa watendaji kusimamia kikamilifu miundombinu ya shule kwa kuzingatia thamani kubwa ya fedha iliyowekezwa,” Amesema Kayombo.
Kayombo amewahimiza wanafunzi wa shule hiyo kusoma kwa bidii ili waweze kufaulu, kuiheshimisha shule yao, na kulinda hadhi yake.
Meneja Ujenzi wa Kanda ya Magharibi wa SUMA JKT CC, Kanali Saul Chimwaga amesema ujenzi huo umezingatia viwango vya juu vya ubora, teknolojia na mifumo ya kisasa ikiwemo ya kuzima moto, ulinzi kwa kutumia kamera za CCTV na matumizi ya biogas.
Meneja wa Mradi huo kutoka kampuni ya Ushauri wa Kitaalam Chuo Kikuu Ardhi (ABECC) Dkt. Kimata Malekela, amesema mradi huo unajumuisha jengo la utawala, madarasa, maabara, ofisi za walimu, ofisi, mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,000 na nyumba 12 za walimu zinazoweza kuchukua walimu 21.
Mkuu wa shule hiyo, Leticia Singo, ameishukuru Serikali kwa kujenga shule bora yenye usajili kamili kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita. Shule hiyo ina wanafunzi 533 wa kidato cha kwanza, tano na sita, na inapokea wanafunzi wa jinsia zote, wakiwemo wenye mahitaji maalum.
Ameeleza kuwa shule hiyo ni jumuishi, ina miundombinu rafiki, mfumo wa biogas kwa shughuli za upishi na uchujaji wa maji taka kwa matumizi ya bustani.
Pia katika shule hiyo kuna darasa janja linalowawezesha wanafunzi kujifunza kupitia vituo vilivyounganishwa kitaifa la katika mfumo wa TEHAMA.