
Na
WyEST
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amezindua Programu ya Utambuzi na Urasimishaji Ujuzi, akieleza kuwa ni utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, toleo la 2023 na maono ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan yanayolenga kutambua na kurasimisha ujuzi unaopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu.

Akizungumza Aprili 22, 2026 jijini Dodoma, Waziri Mkenda amesisitiza kuwa Programu hiyo inakwenda sambamba na malengo ya Dira ya Taifa 2050, ikilenga kuandaa wataalam wenye ujuzi na maarifa kwa uchumi shindani, uzalishaji bora na utatuzi wa changamoto za kijamii.
Amebainisha kuwa, Programu hiyo imefadhiliwa kikamilifu na Serikali na inalenga kuwafikia vijana 80,000 ifikapo Juni 2027, ambapo kati ya Aprili 7- 29, 2026, vijana 14,400 kutoka mikoa 11 wamejiandikisha ili kurasimisha ujuzi wao. 
Waziri Mkenda amemshukuru Mhe. Rais kwa maelekezo yake, kuhakikisha elimu na mafunzo ya ufundi stadi yanakuwa jumuishi na kutoa fursa kwa wale ambao hawakupata mafunzo katika vyuo vya VETA.
Aidha ameipongeza Bodi ya VETA, Menejimenti na watumishi wote kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya. Ameitaka kutekeleza Programu hiyo kwa uwazi na ubora.
Ametoa wito kwa waajiri kuwa tayari kufanya kazi na vijana ambao ujuzi wao utarasimishwa na VETA kupitia Programu ya Mama Samia ya Utambuzi na Urasimishaji Ujuzi.

