Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Wizara hiyo itaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Mageuzi ya Elimu yanayoenga kupata wahitimu wenye ujuzi na mahiri katika nyanja mbalimbali.



Mkenda amesema hayo April 05, 2024 jijini Dodoma akifunga Mkutano wa mwaka wa pamoja na wadau wa Tathimini ya Sekta ya Elimu kwa mwaka 2023/24, ambapo amesema serikali itaendelea kushirikiana na Wadau kuhakikisha inatoa Elimu bora, ikiwemo Elimu ya Amali inayopewa msukumo sasa ili kuwezesha ujuzi kwa Vijana wa Kitanzania.



"Mageuzi tunayoanza nayo yanahitaji ujasiri mkubwa kwa sababu matunda yake hayaonekani harak yana mchakato mrefu matokeo yake yataonekana baada ya muda" Alisema Mkenda.

Ameongeza kuwa Serikali inautambua mchango mkubwa wa Kitaaluma na fedha kutoka kwa wadau mbalimbali wa Maendeleo na kuendelea kusisitiza ushirikiano huo ili kutimiza malengo makubwa ya elimu.



"Nimefurahi kuona Wadau wengi mko hapa na tumekuwa pamoja katika safari hii ya mageuzi ya elimu naamini kupitia Mkutano huu mmejadili na kuweka mipango na mikakati ya pamoja ya kuboresha sekta ya Elimu Nchini, " alisema Mkenda



Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira ya dhati katika kuboresha miundombinu mbalimbali kuanzia Elimu ya Awali hadi Vyuo Vikuu na nia thabit ya kuleta mageuzi katika elimu ili kuhahakikisha hakuna mtoto anakosa fursa ya kupata elimu na ujuzi.



Awali akitoa taarifa kuhusu Mkutano huo Kamishna wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa amesema pamoja na mambo mengine Mkutano huo umeazimia mambo mengi ikiwemo lishe na chakula Shuleni, kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali na Wadau katika utoaji wa mafunzo ya Amali pamoja na kuwekeza katika Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu (STEM) na mazingira.



Kwa niaba ya Wadau wa Maendeleo Mkuu wa Kitengo cha Elimu Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) Dr. Daniel Baheta ameishukuru Menejimenti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikiongozwa na Katibu Mkuu Prof. Carolyne Nombo kwa kushirikisha wadau katika Kongamano hilo