Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko, amesema Serikali imeendelea kuipa kipaumbele sekta ya elimu kwa kutenga takribani asilimia 20 ya Bajeti Kuu kila mwaka kwa ajili ya sekta hiyo.



Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa elimu ulioandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) jijini Dar es Salaam Septemba 24,2025 Dk. Biteko amesema hatua hiyo imeifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika.



Amesema kuwa Serikali inaendelea kujenga mfumo thabiti wa elimu ya kidijitali na kuongeza matumizi ya rasilimali za ndani ili kuimarisha elimu kwa ajili ya sasa na kwa vizazi vijavyo.



Kwa upande wake Mkurugenzi wa TEN/MET, Martha Makala, amesema mtandao huo utaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuimarisha mifumo ya elimu, kuongeza uwekezaji na kuhakikisha kila mtoto nchini anapata elimu kwa ujumuishi, usawa na ubora.



Ametoa pongezi kwa Serikali kufanya mageuzi ya Kisera, mitaala, uboreshaji wa miundombinu ya shule na ongezeko la walimu, akisema hatua hizo ni msingi wa kufanikisha elimu bora na jumuishi nchini.