Serikali ya Tanzania imeendelea kujizatiti katika ujenzi wa miundombinu ya elimu ya juu ili kuongeza fursa za masomo na kukuza ujuzi, ubunifu na utafiti, kwa lengo la kuwaandaa wahitimu wenye uwezo wa kushindana katika soko la ajira kitaifa na kimataifa.



Haya yamebainishwa katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi wa majengo ya Maabara za Sayansi na Skuli ya Kilimo katika Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja, yaliyojengwq na Serikali kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).



Akizungumza Aprili 24, 2026, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amesema mradi huo, utachochea uchumi wa buluu na kuongeza tija katika kilimo na hivyo kuimarisha nafasi ya elimu ya juu katika kuchangia maendeleo ya taifa.



Mhe. Nchimbi amesisitiza kuwa uwekaji wa Jiwe la Msingi unaangazia mafanikio ya Muungano wa Tanzania katika miaka 62 iliyopita, ambao umewezesha kushirikiana zaidi, kuimarisha amani, na kustawisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika pande zote mbili za Muungano.



Makamu wa Rais amemtaka Mshauri Elekezi na Mkandarasi kukamilisha mradi huo kwa wakati, kwa kuzingatia viwango bora, weledi na thamani ya fedha.



Vilevile ametoa rai kwa uongozi wa SUZA kusimamia rasilimali hizo kwa uadilifu na uwazi ili kuhakikisha kuwa miundombinu inayojengwa inawezesha kufikiwa kwa malengo yaliyokusudiwa, ikiwemo kuchochea tafiti na bunifu zinazolenga kutatua changamoto halisi za jamii.