Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba amesema kazi ya uandishi na uchapaji wa mitaala, mihtasari, vitabu vya kiada na Viongozi vya Mwalimu kwa Darasa la kwanza, tatu na kidato cha nne mkondo wa Amali imekamilika.



Akizungumza Machi 15, 2024 Jijini Dar es Salaam wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo ilipofika katika Taasisi hiyo kujionea namna inavyotekekeza majukumu yake ambapo amesema Taasisi hadi kufikia Machi 2024 tayari imepokea 97% ya bajeti iliyotengewa kwa Mwaka wa Fedha 2023/24



Dkt. Komba amesema fedha hizo zimewezesha uandishi wa vitabu vya kiada kwa madarasa yanayotekeleza mtaala mpya, ununuzi wa vifaa vya kuchapa vitabu vya kiada vya wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu kuhusu mtaala mpya.



Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa usambazaji wa nakala laini za vitabu hivyo umefanyika kupitia Maktaba Mtandao ya Taasisi hiyo pamoja na kuchapa nakala zaidi ya milioni nane vya kimacho , maandishi yaliyokuzwa na Breli kwa ajili ya wanafunzi wenye uoni hafifu na wasioona na kwamba usambaji hadi sasa umefikia 64%



Aidha, Dkt Komba amesema kwa upande wa mafunzo kwa wasimamizi na watekelezaji wa mitaala mipya yamefanyika katika makundi matano ambayo ni pamoja na wawezeshaji wa kitaifa, wasimamizi wa utekelezaji, walimu wa elimu ya awali juu ya maudhui na ufundishaji wa somo la English na pia kwa walimu wa Sekondari Mkondo wa Amali wa shule zote 96 zilizoanza kutoa mafunzo hayo.

Ameongeza kuwa taasisi hiyo inaendelea kufanya tathimini na ufatiliaji wa utekelezaji wa mitaala ili kubaini changamoto na kutoa afua stahiki za kuimarisha utekelezaji wa mitaala hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kazini kwa walimu na wasimamizi wa utekelezaji wa mitaala kazi ambayo inaendelea kupitia Mpango Endelevu wa Mafunzo ya Walimu Kazini (MEWAKA)