
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Serera, amesema kuwa sekta ya viwanda ndiyo injini ya uchumi wa taifa, lakini injini hiyo haiwezi kukimbia bila mafuta ya ujuzi.
Akizungumza Oktoba 17, 2025 jijini Dar es Salaam katika mkutano wa VETA, wamiliki wa viwanda, waajiri na wadau wa elimu ya ufundi stadi, Dkt. Serera amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya VETA na sekta ya viwanda si wa hiari, bali ni wajibu wa kitaifa katika kuinua uchumi wa taifa.

Ameeleza kuwa kupitia ushirikiano wa kimkakati kati ya Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, serikali inaendelea kutekeleza mpango wa kujenga uchumi wa viwanda unaotegemea ujuzi wa ndani na kwamba VETA imekuwa nguzo ya mabadiliko ya kiufundi katika sekta za uzalishaji, kilimo, nishati, madini, teknolojia na ujenzi.

Dkt. Serera ametoa wito kwa wamiliki wa viwanda na waajiri kushiriki kikamilifu katika mapinduzi ya ujuzi nchini, akisisitiza umuhimu wa kuunganisha nguvu kati ya sekta ya umma na binafsi ili kuhakikisha mafunzo yanayotolewa na VETA na vyuo vya ufundi yanalingana na teknolojia za kisasa, ikiwemo matumizi ya akili Unde (AI) na viwanda vya kijani.

