Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Fatma Mabrouk Khamis.



Mazungumzo hayo yamefanyika leo, Aprili 10, 2026, jijini Dodoma, yakiwa na lengo la kujitambulisha pamoja na kujifunza namna mbalimbali Wizara ya Elimu inavyotekeleza majukumu yake katika kuendeleza sekta ya elimu nchini.



Katika kikao hicho, Prof. Nombo ameelezea majukumu makuu ya wizara ikiwa ni kutunga Sera na miongozo ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na utafiti kwa lengo la kuwa na miongozo ya kuandaa kujenga jamii yenye maarifa na ujuzi kwa kuzingatia mendeleo ya sayansi na Teknolojia.



Aidha, ameeleza majukumu mengine kuwa ni pamoja na kukuza ubunifu na matumizi ya sayansi na teknolojia nchini, kuweka mazingira wezeshi kwa maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu, pamoja na kuendeleza wataalamu wenye taaluma hizo kwa kushirikiana na wizara na sekta mbalimbali.



Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Fatma Mabrouk Khamis, amesema kuwa wizara yake ina jukumu la kusimamia na kuratibu masuala ya teknolojia ya mawasiliano na ubunifu, pamoja na kupitia na kusimamia sheria za mawasiliano ya kidijitali.