
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeanzisha Programu Maalumu ya Mafunzo ya Tiba Fizikia katika Masuala ya Matibabu, ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha uwezo wa kitaifa wa kutoa huduma za afya zinazotegemea teknolojia ya kisasa.
Akizungumza Septemba 25, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa programu hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema kuwa Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika ununuzi wa vifaa na mitambo ya matibabu ya kisasa katika hospitali mbalimbali nchini.
Hata hivyo, idadi ya wataalamu waliopo ni ndogo, hivyo kuna uhitaji wa kuongeza wataalamu wa ndani wenye ujuzi wa kutumia teknolojia hiyo.
Prof. Nombo alieleza kuwa kutokana na changamoto hiyo, Wizara iliielekeza UDSM kuandaa programu hiyo maalumu ili kuwezesha nchi kuandaa wataalamu wa Tiba Fizikia wa ndani ya nchi, badala ya kutegemea wataalamu kutoka nje.
Programu hiyo itatolewa katika ngazi ya shahada ya kwanza na shahada ya pili, na wahitimu wake watafanya kazi katika vituo vya afya na hospitali mbalimbali nchini.
Aidha, Prof. Nombo alibainisha kuwa programu hiyo itakuwa ya kipekee katika ukanda wa Afrika Mashariki, na hivyo kuvutia wanafunzi kutoka nchi jirani kuja kusoma nchini Tanzania. Hii ni fursa ya kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha elimu ya Tiba Fizikia.
Programu hii imeandaliwa kwa ushirikiano na Tume ya Nguvu za Atomiki pamoja na Taasisi ya Kimataifa ya Masuala ya Nyuklia. Tayari shahada ya kwanza imedahili wanafunzi 20 waliokidhi vigezo, huku shahada ya pili ikiendelea na udahili ambapo hadi sasa wanafunzi saba wameshaandikishwa.
Hatua hii ni ya kihistoria katika kuimarisha rasilimali watu wa ndani na kuhakikisha matumizi ya Tiba Fizikia katika sekta ya afya.