Serikali imewataka Wazazi na walezi kuacha kuficha watoto wenye mahitaji maluum badala yake wawapeleke shule ili kupata haki yao ya Elimu kwa kuwa sasa kuna fursa na mazingira wezeshi kwa wao kupata elimu.



Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe Machi 04, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa Halfa ya utoaji vifaa saidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum wa shule za Sekondari vilivyotolewa na Wizara na wadau mbalimbali.



Prof. Mdoe ameongeza kuwa serikali kila mwaka inatenga fedha katika bajeti yake kwa ajili ya kununua vifaa hivyo ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23 ilitengwa fedha ambayo imewezesha kununua viti mwendo vipatavyo 530, vitabu vya kutosheleza vya nukta nundu, maandishi makubwa pamoja na vifaa vya kusaidia usikivu.



“Takwimu zinaonyesha kuanzia elimu ya awali mpaka kidato cha sita kuna wanafunzi wenye mahitaji maalum zaidi ya elfu 92 ambapo kwa Dar es Salaam tu kuna wanafunzi zaidi ya 5000 ambao wanamahitaji mbalimbali ikiwemo Viti mwendo, Vifaa vya kuongeza usikivu, vitabu vya breli na kompyuta” amesema Prof. Mdoe



Ameongeza kuwa pamoja na serikali kutenga fedha na kununua vifaa hivyo bado havitoshelezi n hivyo kutoa wito kwa wadau kuendelea kujitokeza kushirikiana na Serijali kuhakikisha mazingira wezeshi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum yanapatikana.



Naibu Katibu Mkuu huyo amewashukuru kampuni ya LM international, Kampuni ya Sigara pamoja na Sloam International kutoka Korea Kusini kwa kushirikiana na Serikali kutoa vifaa saidizi kwa shule za sekondari Pugu, Janwani na Dodoma, vifaa hivyo ni pamoja na Viti mwendo, Kompyuta Mpakato, Vishikwambi, mashine ya kufulia, Projekta na magodoro