Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika elimu ya ufundi nchini ikiwemo kugharimia chakula na mafunzo kwa vitendo viwandani kwa maelfu ya wanafunzi, ili kuzalisha rasilimaliwatu yenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuchochea maendeleo ya Taifa.



Hayo yamesemwa Januari 8, 2026 mkoani Songwe na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi, alipomwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, kama Mgeni Rasmi katika Mahafali ya Kumi na Tisa (19), Duru ya Tatu (3) ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Kampasi ya Songwe.



Profesa Mushi amesema kuwa Serikali itaendelea kugharamia elimu ya ufundi katika mwaka wa fedha 2025/2026 ikiwemo kutoa huduma ya chakula kwa wanafunzi 18,316 katika taasisi mbalimbali za elimu ya ufundi nchini pamoja na kugharamia mafunzo kwa vitendo viwandani (Industrial Practical Training – IPT) kwa wanafunzi 2,085.



Ameeleza kuwa jitihada hizo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha Taifa linakuwa na wataalamu wa fani za amali wenye uwezo wa kuchachua maendeleo ya kiuchumi na kusaidia kutatua changamoto za jamii.



Akizungumza katika mahafali hayo, Profesa Mushi amewapongeza wahitimu wa Stashahada ya Uhandisi Ujenzi na wahitimu wa fani ya ufundi bomba ngazi ya pili, akisema kuwa elimu waliyoipata ni hazina kubwa kwao binafsi, familia zao na Taifa kwa ujumla.