Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Profesa Preksedis Ndomba, amesema kuwa Taasisi hiyo imejikita katika dhana ya ufundishaji inayotilia mkazo mafunzo kwa vitendo pamoja na ziara za mafunzo viwandani.



Akizungumza jijini Dar es Salaam tarehe 5 Disemba 2025, katika duru ya kwanza ya Mahafali ya 19 ya Taasisi hiyo, Prof. Ndomba ameeleza kuwa dhana hiyo inahimiza kauli mbiu ya kiwanda ndio darasani aesema hatua hiyo imewasaidia wanafunzi kuwa wabunifu na kufikia viwango vya kuanzisha makampuni.



Aidha Prof. Ndomba amewapongeza wahitimu wote kwa mafanikio makubwa yaliyotokana na ubunifu wao, akisisitiza kuwa mchango wao ni muhimu katika kuchochea maendeleo ya taifa katika nyanja mbalimbali kama vile uchumi na kijamii.



Katika duru ya kwanza ya mahafali hayo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf mkenda amewatunuku vyeti jumla ya wahitimu 1,341 katika ngazi mbalimbali za Astashahada, Stashahada, Shahada na Shahada ya Uzamivu katika nyanja za Sayansi na Teknolojia. Kati ya hao, wanaume ni 1,003 na wanawake 338.