
Serikali imesisitiza kuwa maboresho makubwa yanayoendelea katika sekta ya elimu yanahitaji uwekezaji wa kutosha wa rasilimali fedha na watu ili utekelezaji wake uwe wa ufanisi na wenye matokeo chanya.
Kauli hiyo imetolewa Jijini Dar es Salaam, Septemba 24, 2025 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Kujadili Ubora na uwekezaji katika sekta ya Elimu ulioandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET).
Prof. Nombo amesema kuwa Serikali imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu ili kuhakikisha rasilimali muhimu zinapatikana kwa ajili ya kuendeleza sekta hiyo na amesisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa sera na mikakati inayolenga kuhakikisha elimu inatoa maarifa na ujuzi stahiki kwa wanafunzi.
Aidha, Prof. Nombo amebainisha kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika kuimarisha mifumo ya utoaji elimu pamoja na kuongeza rasilimali fedha. Hata hivyo, amekiri kuwa bado kuna uhitaji wa rasilimali za kifedha, kitaalamu na kitaaluma ili kufikia malengo kusudiwa.
Mkutano huo umeweka jukwaa la kujadili kwa kina changamoto na fursa zilizopo katika sekta ya elimu, huku wadau wakitakiwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuleta mageuzi ya kweli yanayolenga kuandaa kizazi chenye maarifa, ujuzi na uwezo wa kushindana katika soko la ajira la kimataifa.