
40 wanufaika na ufadhili
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema kuwa ushirikiano ulioanzishwa kati ya Taasisi ya Mo Dewji, Kampuni ya Kerry Group, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) utasaidia kuwaunganisha vijana na viwanda wapate ujuzi.
Prof. Nombo amesema hayo Septemba 25, 2025, jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa Mpango wa Ufadhili wa Mo-Krry Scholarship. Alieleza kuwa ingawa wahitimu wanapata maarifa ya kitaaluma vyuoni, mazingira ya viwanda na teknolojia hubadilika kwa kasi, hivyo kuna umuhimu wa kuwapa vijana fursa ya kujifunza kwa vitendo.
Mpango huu unalenga kuwajengea uwezo wahitimu wa masomo ya Sayansi ya Chakula na Kilimo kutoka vyuo mbalimbali nchini. Kupitia ufadhili huu, wahitimu wataanza kwa mafunzo ya nadharia katika UDSM na SUA kwa kipindi cha miezi minne, wakijifunza mbinu za kisasa na maarifa ya kitaalamu yanayohusiana na sekta ya kilimo na chakula.
Baada ya kukamilisha mafunzo ya darasani, washiriki wa mpango huu watapelekwa katika viwanda vya Mo Dewji kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo. Hatua hii inalenga kuwapa uzoefu wa moja kwa moja katika mazingira ya kazi, ili kuongeza ujuzi na kuwaandaa kwa ajira au ujasiriamali katika sekta husika.
Mwaka huu jumla ya wanafunzi 40 watanufaika na mpango huo, ambapo Tanzania inatumika kama nchi ya majaribio. Aidha baada ya tathmini ya awali, Mo-Krry Scholarship inatarajiwa kutekelezwa katika nchi nyingine za Afrika Mashariki, ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuwezesha vijana wa Afrika kuchangia kikamilifu katika maendeleo endelevu ya barani humo.