Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Phillipo Sanga, amesema kuwa Taasisi hiyo imejipanga kuongoza kwa ubunifu na dira pana katika kupanua wigo wa fursa za Elimu Msingi Nje ya Mfumo Rasmi nchini.



Akizungumza Septemba 19, 2025, katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kisomo Kimataifa na Juma la Elimu ya Watu Wazima, Prof. Sanga alibainisha kuwa TEWW itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi mkubwa sambamba na kuongeza matumizi ya teknolojia kama nyenzo muhimu ya kuleta mapinduzi katika utoaji wa elimu kwa watu wazima.



"Tutaongeza wigo wa kuwafikia Watanzania wote, hususan makundi yaliyoko pembezoni ambayo kwa muda mrefu hayajapata huduma ya elimu stahiki,” alisisitiza Prof. Sanga.

 

Kwa mujibu wa Prof. Sanga, hatua hizi ni sehemu ya jitihada za kitaifa kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki ya msingi ya kujua kusoma, kuandika na kuhesabu msingi wa ushiriki kamili katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya taifa.