
Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi CCM Taifa, Fadhil Rajabu Maganya, amesema kuwa ujenzi wa VETA nchini pamoja na uwekaji vifaa na samani za kisasa katika vyuo hivyo itawezesha vijana kujifunza kwa vitendo na kupata ujuzi wa kujiajiri.

Mwenyekiti Maganya amesema hayo tarehe 17 Januari 2026 jijini Dodoma wakati wa ziara ya viongozi wa Umoja huo kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM, Maganya alisema ujenzi wa VETA 65 za wilaya na moja ya mkoa wa Songwe ni hatua ya kujivunia inayolenga kuongeza umahiri wa vijana ili waweze kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Mohamed Omar, akizungumza kwa niaba ya Waziri alisema Serikali inaendelea kutekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ili kuimarisha elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa lengo la kuwaandaa vijana kuwa wabunifu, wazalishaji na washindani katika uchumi wa kitaifa na kimataifa.


