
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema kuwa Wizara itaendelea kutekeleza maagizo ya Serikali na kushirikiana kwa karibu na viongozi mbalimbali ili kuimarisha na kuboresha sekta ya elimu nchini.

Prof. Nombo ametoa kauli hiyo tarehe 15 Desemba 2025 mkoani Kagera, wakati akizungumza katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa Kampasi ya Kagera ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), inayotekelezwa na Serikali kupitia mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET).

Amesisitiza kuwa ujenzi wa kampasi hiyo ni kielelezo cha dhati cha utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuwekeza katika elimu ya juu na kusogeza huduma za elimu karibu na wananchi, ili kuongeza fursa na kuimarisha upatikanaji wa elimu bora nchini.

