
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Daniel Mushi, amesema kuwa Maadhimisho ya Siku ya Kisomo Kimataifa na Juma la Elimu ya Watu Wazima yamechochea utekelezaji wa malengo ya Elimu ya Watu Wazima na Nje ya Mfumo Rasmi.
Prof. Mushi ameeleza hayo Septemba 19, 2025 mkoani Katavi katika Kilele cha Maadhimisho hayo, ambapo amesema kuwa yamewapa wanajamii fursa ya kushiriki kikamilifu, na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha malengo ya Elimu ya Watu Wazima na Nje ya Mfumo Rasmi.
Aidha, Prof. Mushi amesema wadau mbalimbali wamepata nafasi ya kujadili kwa kina mada muhimu, ikiwemo matumizi ya teknolojia katika utoaji wa elimu ya watu wazima, malezi bora kwa watoto, pamoja na mbinu za kujenga stadi na ujuzi kwa vijana.
Maadhimisho hayo yamehusisha maonesho ya bidhaa na huduma kutoka kwa wanakisomo, kongamano la kitaifa, pamoja na kikao kazi kilichowakutanisha Maafisa Elimu kutoka maeneo mbalimbali nchini.