Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Elimu 2025/26-2029/30 imetenga zaidi ya asilimia 14 ya rasilimali za ndani kwa ajili ya miradi ya elimu ili kuendeleza elimu jumuishi, yenye usawa na ubora kwa wote.



Akizungumza jijini Dar es Salaam Septemba 26, 2025, wakati wa kufunga Mkutano wa Kimataifa wa Elimu, Katibu Mkuu Prof. Carolyne Nombo amesema kuwa uwekezaji kwa walimu ni msingi wa elimu bora na kwamba Serikali imeanzisha Bodi ya Walimu kwa ajili ya ushauri, maadili ya kitaaluma, na mafunzo endelevu.



Prof. Nombo ameongeza kuwa walimu wanapatiwa mafunzo ya TEHAMA na stadi mbalimbali za ufundishaji ili kwenda sambamba na mitaala inayobadilika na kuwaandaa wanafunzi kwa soko la ajira linalobadilika Kwa kasi huku akisisitiza kuwa usawa wa kijinsia na ujumuishi vitabaki kuwa kiini cha ajenda ya elimu.



Mratibu wa Taifa wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) Bi. Martha Makala amesema nchi zimekubaliana kuongeza matumizi ya rasilimali za ndani ili kufadhili elimu kwa njia endelevu, hata wakati wa misukosuko ya kiuchumi.



Aidha, umewekwa msisitizo kuwekeza katika elimu ya awali, kuwajumuisha vijana na makundi yaliyotengwa katika sera za elimu, na kutambua nafasi ya teknolojia na akili bandia.



Tracy Osuo kutoka Mastercard Foundation amehimiza kuimarisha ushirikiano wa sekta binafsi, wafadhili na Serikali ili kuimarisha maendeleo ya kitaaluma.