
Mshairi Maarufu Duniani Abdilatif Abdallah kutoka nchini Ujerumani anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika hafla ya Nne ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu mwaka 2026.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Aprili 8, 2026 Jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa Abdilatif Abdallah ana asili ya Afrika Mashariki na si mgeni kwa Tanzania kwani aliwahi kuishi na kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka 15.

"ujio wake ni heshima kubwa kwa Tanzania na mchango wake katika kukuza kazi za uandishi bunifu utakuwa na manufaa kwa mataifa ya Afrika Mashariki," ameongeza Prof Mkenda.
Aidha, ameongeza kuwa kabla ya hafla ya utoaji tuzo kutakuwa na mjadala wa kitaaluma utakaoshirikisha waandishi bunifu maarufu wa Tanzania pamoja na wageni mashuhuri ambao ni Dkt. Aida Mutenyo kutoka Uganda na Bw. Ferdinand Ndahayo kutoka Rwanda.
Tukio hili litatoa fursa ya kubadilishana mawazo na kuimarisha nafasi ya Kiswahili na fasihi bunifu katika ukanda wa Afrika Mashariki na kimataifa

