
Serikali imesema itaendelea kuwezesha vijana kupata ujuzi wa kisasa katika sekta ya kilimo ambapo ni hatua muhimu ya kuimarisha uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao na kukuza uchumi wa taifa.

Kauli hiyo imetolewa leo Machi 5, 2026 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, akimwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, katika uzinduzi wa Mradi wa Ujasiriamali wa Vijana kwa Mustakabali wa Chakula na Kilimo (YEFFA) katika Chuo cha VETA Kihonda, mkoani Morogoro.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Wanu amesema mradi huo unalenga kuwapa vijana maarifa na stadi muhimu katika sekta ya kilimo hususan katika maeneo ya ufundi wa zana za kilimo, teknolojia ya umwagiliaji na teknolojia za uhifadhi wa mazao baada ya mavuno.

Amesema matumizi sahihi ya teknolojia hizo yataongeza tija katika uzalishaji na kusaidia kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, hali itakayochangia kukuza uchumi na ustawi wa wananchi.

Aidha, ameongeza kuwa Serikali imeweka mkazo mkubwa katika kuifanya sekta ya kilimo kuwa ya kisasa na yenye tija kupitia utoaji mafunzo ya ujuzi ili kuwa na rasilimali watu itakayofanikisha hayo.

Amesema tangu kuasisiwa kwa taifa, sekta ya kilimo imeendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa nchi kwa kuajiri zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania hivyo sekta ya elimu pia inaweka mkazo utojii mafunzo katoka kilimo na hata ufugaji.

Kwa mujibu wa Mhe. Wanu, ili sekta hiyo iweze kushindana kikanda na kimataifa ni lazima iendeshwe na nguvu kazi yenye ujuzi, ubunifu na maarifa ya kibiashara, hasa katika kipindi ambacho kilimo kinaendelea kubadilika kutokana na matumizi ya zana na mitambo ya kisasa, mifumo ya umwagiliaji yenye ufanisi na teknolojia za kuhifadhi mazao baada ya mavuno.

“Kilimo cha sasa si cha jembe la mkono pekee bali ni kilimo kinachotumia teknolojia, kinachoongeza thamani ya mazao na kinacholenga biashara, hivyo vijana wanapaswa kuandaliwa kwa ujuzi utakaowawezesha kushiriki kikamilifu katika mnyororo mzima wa thamani katika kilimo,” amesema Mhe. Wanu


