Chuo Kishiriki cha  Elimu Dar es Salaam kwa mara ya kwanza mwaka huu kinaanza kutoa Shahada ya Uzamivu katika Lugha za Kiafrika ( PhD in  African Languages)



Hayo yamesemwa Machi 14, 2026 jijini Dar es Salaam na Rasi wa Chuo hicho Prof. Stephen Maluka wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo.



Amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya wataalamu kugundua lugha za kiafrika kuwa hatarini kutoweka, kutokuwepo tafiti nyingi katika lugha hizo na  vyuo katika nchi nyingi za Kiafrika kutoa shahada za uzamivu katika lugha za kigeni pekee.



Aidha Prof. Maluka aliieleza Kamati kuwa Chuo hicho kimefanikiwa  katika ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa kuwa na Kitengo cha Elimu Maalum kinachohakikisha kuwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wanatambuliwa na kupewa huduma stahiki kulingana na uhitaji wao.



Ameongeza kuwa kwa kushirikiana na wadau pamoja na Serikali wamepata vifaa vya kufundishia ka kujifunzia kama kompyuta, vinasa sauti, mashine ya nukta nundu, mashine ya kusaidia usikivu, vishikwambi, fimbo maalum za kutembelea na miguu ya bandia.



"Tuna wanafunzi 48 wenye mahitaji maalum na tunahakikisha kuna miundombinu rafiki kwa wanafunzi hao," amesisitiza Rasi wa Chuo

Akizungumzia ujenzi wa miundombinu unaofanywa na Serikali kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya kiuchumi (HEET) Prof. Maluka amesema DUCE ilitengewa kiasi cha Dola la Kimarekani zipatazo milioni na Nane kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, kuboresha mitaala ili iendane na mahitaji ya soko la ajira.



Amesema kupitia fedha hizo Chuo kinajenga majengo mawili moja likiwa la Insia na Sayansi za Jamii na jengo la Shahada za Uzamili lenye maabara za sayansi, ujenzi wake ukiwa umefikia asilimia 85.