Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo wamekipongeza Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam kwa kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kusoma bila changamoto yoyote.



Pongezi hizo zimetolewa jijini Dar es Salaam Machi 14, 2026 mara baada ya wajumbe hao kukamilisha ziara ya kukagua maendeleo ya Ujenzi wa miundombinu chuoni hapo unaofanywa na Serikali kupitia Maradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi ( HEET)



Akizungumza katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo Mhe. Husna Sekiboko amesisitiza ujenzi katika maeneo ya elimu kuzingatia wanafunzi wenye mahitaji maalum huku akipongeza uongozi wa Chuo na Wizara kwa usimamizi mzuri wa Miradi ya elimu.



Mhe. Sekiboka ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha fedha za utekelezaji wa miradi zinafika kwa wakati na ujenzi unafanyika.



"Tunaipongeza Serikali, kote tulipopita hatujapacha changamoto ya fedha kutofika niwaombe sasa muendelee kusimamia miradi hii ikamilike kwa wakati",amesisitiza Mhe. Sekiboko.



Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda ameihakikishia Kamati kuwa Wizara anayoisimamia itaendelea kufanya kazi kwa bidii huku ikiongeza umakini katika na utekelezaji na usimamizi wa miradi ya elimu.



Akizungumzia ujenzi wa miundombinu rafiki kwa wenye mahitaji maalum amesema ni maelekezo ya Rais Samia na kwamba Wizara imezingatia hili kuanzia kwenye ujenzi wa miundombinu, walimu na upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia