
Serikali imesema itaendea kuweka mkazo katika kuimarisha maslahi, ushiriki na mazingira ya kazi kwa walimu wanawake na walimu wenye ulemavu ikiwa ni sehemu ya juhudi za kujenga mfumo jumuishi wa elimu unaotoa fursa sawa kwa wote.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma Februari 6, 2026 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Wanu Hafidh Ameir wakati wa ufunguzi wa kikao cha Wawakilishi wa Walimu Wanawake na Walimu wenye ulemavu kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara.

Mhe. Wanu amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali imenunua na kusambaza vifaa maalumu vya kielimu vya kidigitali na saidizi kwa walimu, wakufunzi na walimu tarajali wenye ulemavu, ambapo walimu 1,055 wa shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu nchini wamenufaika na vifaa hivyo vyenye thamani ya Shilingi bilioni 5.3

Akizungumzia kikao hicho Mhe. Wanu amesema wawakilishi wa Walimu watapatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo walimu wanawake na walimu wenye ulemavu ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mhe. Wanu amekipongeza Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa kuendelea kuwaunganisha walimu nchini, wakiwemo walimu wenye ulemavu na wanawake, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa karibu na Serikali, taasisi na mashirika mbalimbali yanayojihusisha na masuala ya watu wenye ulemavu na wanawake.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ndugu Suleiman Ikomba, amesema walimu ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa, ambapo kupitia elimu ndipo jamii na taifa kwa ujumla hujengwa na maendeleo endelevu kupatikana.


